Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akizungumza na baadhi ya wananchi wa Lindi aliowaalika kwenye futari mara baada ya kuwafuturisha nyumbani kwake,Lindi Mjini jana.
Mke wa Rais Mama Salma Kkwete akisalimiana na baadhi ya akinamama aliofuturu nao nyumbani kwake Lindi Mjini,jana.
Baadhi ya wananchi wa Lindi Mjini walioalikwa kufuturu nyumbani kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakisikiliza mawaidha yaliyokuwa yakitolewa baada kufuturu.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiaagana na Shehe Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi Al Haj Mohamed Said Mshangani baada ya kufuturu nyumbani kwa Mama Salma huko Lindi Mjini tarehe 27.7.2013. PICHA NA JOHN LUKUWI
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa mkoa wa Lindi kuishi maisha ya upendo, ushirikiano, umoja na kuwasaidia watu wasiojiweza kwa kufanya hivyo watapata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Mama Kikwete ametoa wito huo jana wakati wa futari ya pamoja iliyowajumuisha watu wa makundi mbalimbali kutoka mkoa huo.
Mama Kikwete alisema upendo ukiwepo ndani ya jamii watu wataishi maisha ya furaha na amani huku wakisaidiana kwa kupeana vitu vichache walivyonavyo.
'Tuwe watu wa kuishi maisha ya kumpendeza Mwenyezi Mungu siyo wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani peke yake bali katika maisha yetu yote, tusali swala tano na kuamka usiku wa manane muda ambao Dunia imetulia, kila mtu anakuwa amelala.
Muombe Mwenyezi Mungu akuamshe muda huo ili uweze kusali bila kusahau kumshukuru kwa kukupa uhai na umri uliofikia na hata kama utakufa muda huo hautakuwa na hofu kwani umeshatengeneza mahusiano yako na Mungu", alisema Mama Kikwete.
Aliendelea kusema ni muhimu kwa muumini wa dini ya Kiislamu kukumbuka kusali, kufunga na kusaidia watu wenye mahitaji maalum kwa kufanya hivyo atakuwa anajilinda na kujitengenezea maisha mema pindi atakapokufa.
Mama Kikwete pia alisisitiza umuhimu wa kutunza amani ya nchi na kuwataka wakazi wa mkoa huo wanapokuwa kwenye mikusanyiko mbalimbali ikiwa ni pamoja na misikitini, makanisani kwenye sherehe na misiba wahubiri umuhimu wa amani kwani mahali penye vita hakuna umoja, ushirikiano na upendo.
Hivi sasa waumini wa dini ya Kiislamu wako katika kumi la pili la kufunga ambalo ni la msamaha kama alivyosema Mtume Swalallahu Alayhi Wassalam (S.A.W) hivyo basi kwa wale wanaofunga wanatakiwa kujikita zaidi kufanya mambo mazuri kwa watu ikiwa ni pamoja na kulisha wengine kwani ukimpa kula na kunywa mwenzako Mwenyezi Mungu anakulipa zaidi.
ConversionConversion EmoticonEmoticon