MICHUZI: KAULI YA JESHI LA MAGEREZA JUU YA MAAFISA WAKE WANNE WALIOKAMATWA NA NYARA ZA SERIKALI

MICHUZI
Libeneke la Globu ya Jamii 
thumbnail KAULI YA JESHI LA MAGEREZA JUU YA MAAFISA WAKE WANNE WALIOKAMATWA NA NYARA ZA SERIKALI
Jul 26th 2013, 14:25, by noreply@blogger.com (MUHIDIN MICHUZI)

Jeshi la Magereza Tanzania Bara linapenda kuufahamisha Umma kwamba mnamo tarehe 23 Julai, 2013 Maafisa wanne ambao ni Mrakibu Msaidizi wa Magereza Joseph Kimaro, Sajenti Ketto Ramadhani, Koplo Silyvester Dionice na Wada Richard Barick wa Gereza Kiteto Mkoa wa Manyara walikamatwa na askari wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kati wakiwa na gari la Jeshi la Magereza pamoja na silaha likiwa limepakia nyara za serikali. 

Dereva wa gari hilo Sajenti Ketto Ramadhan alitoroka na kutelekeza gari hilo na Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu na maadili ya Jeshi la Magereza pamoja na sheria za uwindaji wa wanyama pori. Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Magereza limechukua hatua zifuatazo:-

i - Askari 3 waliohusika wamefukuzwa kazi kwa kosa la kwenda kinyume na maadili ya Jeshi la Magereza na watafikishwa Mahakamani baada ya upelelezi wa Polisi kukamilika.

ii - Afisa Mrakibu Msaidizi wa Magereza Joseph Kimaro amefunguliwa mashtaka ya kinidhamu na kusimamishwa kazi kwa kosa la kwenda kinyume na maadili ya Jeshi la Magereza hadi maamuzi ya Mamlaka ya kinidhamu inayomuhusu yeye (Disciplinary authority) itakapotoa maamuzi dhidi yake. Kwa sasa amezuiliwa Kituo cha Polisi Babati kusubiri kufikishwa Mahakamani upelelezi wa Polisi utakapokamilika.

iii - Mkuu wa Gereza Kiteto Mrakibu wa Magereza Ally Ramadhani Sauko kwa kutumia madaraka yake vibaya hivyo amevuliwa uongozi na kuhamishiwa Ofisi ya Mkuu wa Magereza Manyara, akisubiri maamuzi ya Mamlaka ya kinidhamu inayomuhusu yeye (Disciplinary authority) kufuatia mashtaka ya kinidhamu yaliyofunguliwa dhidi yake.

Imetolewa na Kitengo cha Habari 
Ofisi ya Makao Makuu ya Magereza Tanzania Bara

You are receiving this email because you subscribed to this feed at blogtrottr.com.

If you no longer wish to receive these emails, you can unsubscribe from this feed, or manage all your subscriptions
Previous
Next Post »